Thursday, 16 March 2017

KKKT: TAZAMENI TUNAPANDA KWENDA YERUSALEMU

SIKU YA BWANA YA SABA KABLA YA PASAKA
ZABURI 123:1 - 4, 2KORINTHO 11: 23 - 30, *LUKA 18: 31 - 34
TAREHE 26/02/2017

"Nanyi mnafahamu kwamba, Mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au kwa dhahabu, mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu, bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana - kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo" (1Petro 1:18 - 19)

UTANGULIZI

  • Mungu aliye mwema sana kwetu kwa neema yake leo ametupa kibalil cha kulitafakari neno lake toka Luka 18: 31 - 34  linalozungumzia safari yake ya kwenda Yerusalemu
  • Safari ya Yerusalemu ni muhimu sana kwetu na kwa Yesu Kristo. Kwa Yesu kwa sababu anakamilisha lengo lake la kimkomboa mwanadamu. Na Kwetu sisi wanadamu ni muhimu sana sababu kwa kukamilika kwa lengo la Yesu sisi tunakombolewa toka katika mikono ya shetani.
  • katika safari hii ya kwenda Yerusalemu ndipo Yesu anatabiri kwa mara ya tatu juu ya mateso yake na kifo chake na ufufuko wake.
  • Habari hii pia inapatikana katika injili nyingine (Mathayo 20;17 - 19, Marko 10:32 - 34) ambapo katika habari hii tunajifunza mambo yafuatayo

1. UHUSIANO MZURI NA MUNGU UNATUFUNULIA MAMBO YATAKAYOTOKEA.

  • Yesu alipokuwa akiwahudumia na kuwafundisha watu wengi ulipofika wakati wa kutaka kusema yatakayotokea baadae aliwatenga faraghani wanafunzi wake na kuwaeleza habari za yeye kwenda Yerusalemu na kuteswa, kuuwawa na kufufuka.
  • Tunapaswa sisi wote tuliochaguliwa na Yesu kwa neema yake tutafute ukaribu na uhusiano mzuri naye kwa nia ya toba kama alivyosema katika mathayo 4:17 "Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri akisema, tubuni kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia" ili tuweze kupatiwa siri za kimbingu tuweze kumshinda shetani na kuurithi uzima wa milele.

2. NGUVU NA UMAARUFU WETU USIPOFUSHE MACHO NA MASIKIO YETU YA KIROHO

  • Wanafunzi walipoelezwa habari ya Mambo yatakayotokea Yerusalemu tunaambiwa kuwa hawakuelewa maneno hayo hata kidogo.
  • Walikuwa karibu na Yesu sawa, walikuwa na imani sawa, lakini hawakuelewa neno lolote
Swali la kujiuliza:-
  • Kwanini Hawakuelewa? Jibu lake kulingana na kifungu tulichosoma unaweza kunijibu kwa sababu yalikuwa yamefichwa kwao. Ni sawa
Swali lingine la kujiuliza hapa, Kwa nini yalifichwa kwao? 
  • Swali hili linahitaji Muda kulitafakari na kumuomba Mungu akufunulie. Yaweza kuwa Mungu alitaka yatakapotokea hayo wakumbuke na utukufu wake uwe mkuu ama sababu ya pili ianatokana na wanafunzi wake.
  • Kwanza wanafunzi kwa kuona mambo yaliyokuwa yanafanywa na Yesu, nguvu alizotumia, na umaarufu walioupata kwa kipindi kile walijua wakifika Yerusalemu watakuwa watawala, ndio maana Yakobo na Yohana walimuomba Yesu wakae mkono wa kuume na mwingine mkono wa kushoto na wale wenzao walikuwa na mawazo kama hayo na waliposikia wakakasirika (Marko 10:35 - 42)
  • Pili hawakuwa tayari kuamini wala kukubaliana na ukweli wa mateso yatakayotokea "Petro akamchukua akaanza kumkemea akisema, hasha, Bwana, hayatakupata"(Mt 16:22)
Maswali ya kujiuliza sisi wa leo
  1. Je, ni mara ngapi nguvu na umaarufu  wetu umetufanya tusikubali kweli ya neno la Mungu?
  2. Je, ni mara ngapi mambo ya kidunia yametufanya tushindwe kuamini kweli ya neno la Mungu?
  • Yawezekana kabisa kuwa Mungu anaongea nasi mara kwa mara lakini tunashindwa kumuelewa wala kumuamini kwa sababu tu ya mawazo yetu ya kibinadamu yanayofanya macho yetu ya kiroho yasione wala masikio yetu yasisikie
  • Yawezekana ni nguvu zetu, umaarufu wetu, utajiri wetu, elimu yetu, cheo chetu ndivyo vinavyotufanya tusielewe kweli ya neno la Mungu.
  • Vitu vyote nilivyotaja hapa ni vitu vya baraka sana kwetu na kwa kanisa kama vikitumika kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
  • Nguvu uliyonayo, umaarufu ulionao, utajiri ulio nao, elimu uliyo nayo, cheo ulichonacho badala ya kujivuna navyo, umuulize Mungu anataka uvifanyie nini kwa ajili ya utukufu wake
  • Vitu hivi tukivifanya si chochote mbele za Mungu na kutambua kuwa Mungu ndie asili ya kila kitu basi itakuwa rahisi kwetu  kuisikia sauti ya Mungu na kuielewa.

3. MATATIZO YASIKUONDOE KWENYE LENGO

  • Lengo la Yesu Kwenda Yerusalemu ilikuwa ni kuumkomboa mwanadamu, japo alitambua atafanyiwa dhihaka, atatendewa jeuri, atatemewa mate, atapigwa mijeledi, atauwawa, hayo yote hayakuweza kufanikiwa kumuondoa Yesu kwenye lengo lake la kumkomboa mwanadamu, alitambua baada ya hayo atashinda kwa kiasi kikubwa kwa kufufuka na kumpatia ukombozi mwanadamu aliyeasi na kutengwa mbali na uso wa Mungu.
  • Wakristo wa leo tunayosafari ya kuuendea uzima wa milele kwa kupitia wokovu wa milele kwa kumwamini Yesu  aliyetupatia ukombozi kwa njia ya msalaba "naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii" (Ebr 5:9)
  • Safari hii ya kuelekea uzima wa milele inatupatia maisha ya baraka hapa duniani na baadae uzima wa milele "ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba,na ndugu waume, na ndugu wake, na mama na watoto, au mashamba, pamoja na udhia na katika ulimwengu ujao uzima wa milele"(Mk 10:30)
  • Safari hii nayo ina mateso yake, Je mateso hayo yamekuondoa kwenye lengo? Mateso haya yanaweza kuwa kunyanyaswa, kuonewa, kudhalilishwa, kuchukiwa, kupigwa na hata magonjwa. haya yote yanaweza kuwepo lakini yasikuyumbishe imani yako, wewe ngangana tu kwenye lengo la kuuridhi uzima wa milele.

4.HITIMISHO

  1. Je, kuna kitu ambacho kimekutenga wewe mbali na uso wa Yesu na usiweze  kusikia sauti yaku?
  2. Je, kuna hali yoyote ya kuviangalia vitu vya dunia hii vinavyoharibika na kuacha kusikia sauti ya Mungu?
  3. Je kuna mambo yaliyotokea ambayo yameondoa kwenye lengo lako la uzima wa milele?

Tumuombe Mungu kwa neema yake tuweze kuboresha uhusiano wetu na yeye na kuyatafuta mapenzi yake ili tuweze kusikia na kuelewa neno lake na kusimama kwenye lengo letu la kupata uzima wa milele.
AMEN.

KKKT: NENO LA MUNGU LINA NGUVU

SIKU YA BWANA YA 8 KABLA YA PASAKA
ZABURI 118: 23 - 29, MARKO 4:1- 9, *YEREMIA 23:24 - 29

TAREHE 19/02/2017

" Maana neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote, ukatao kuwili, tena lachoma hata kugawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomondani yake, tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo"(Ebr 4:12)

UTANGULIZI

  • Ashukuriwe Mungu ambaye kwa neema yake leo ametupa kujifunza neno lake, huku tukikumbushwa kuwa "Neno la Mungu lina Nguvu"
  • Neno la Mungu si jambo fulani lililoandikwa au kusemwa tu, bali ni jambo lililofanya mambo, ndani ya neno mlikuwa na nguvu ya Mungu.
  • Neno la Mungu ni nafsi iliyo hai. (Yohana 1:1 - 4,14)
  • Neno la Mungu lililosemwa liliandikwa  na neno ni nafsi ya Yesu na ni hai nalo linafanya kazi (Ebr 4:12)
  • Na leo tunaangalia neno kutoka Yeremia 23:24 - 29, ambayo ni sehemu ya nne katika mfululizo wa mafundisho juu ya nabii wa uongo katika kitabu hiki cha Yeremia mlango wa 23, ambapo sehemu hizo ni
  • Sehemu ya kwanza 23:9 - 12
  • Sehemu ya pili 23:13 - 15
  • Sehemu ya tatu 23:16 - 22
  • Sehemu ya nne  23:23 - 32
  • Sehemu ya tano 23:33 - 40
  • Katika sehemu hii ya nne mwandishi anatuonyesha juu ya uwepo wa manabii wa uongo ns msnsbii wa ukweli
  • Manabii wa uongo wanaongozwa na ndoto na akili zao wakizingatia mazoea na miujiza 
  • Manabii wa ukweli wanaongozwa kwa neno la Mungu
  • Katika soo hili tunaona mambo haya muhimu

1. MUNGU YUPO KILA MAHALI

  • Hakuna mwanadamu anayeweza kujificha Mungu asimuone awe ni mtu mwema au asie mwema, wote anawaona.
  • Anayetenda mabaya au mema ajue kuwa Mungu anamuona na atalipwa kulingana na matendo yake hivyo mtu asijifariji katika kutenda mabaya kisa tu hajaona Mungu anamuadhibu waziwazi. jua unaonekana na utalipwa kulingana na mwenendo wako

2. SI KILA ANAYETAJA JINA LA MUNGU ANAFANYA MAPENZI YA MUNGU

  • Mungu anasema manabii wa uongo wanatumia jina lake kuendeleza uongo wao ili waweze kukubalika mbele za watu, wanayasema maneno ya Mungu huku wakijidanganya wenyewe na kuwadanya wengine wafanane nao
  • Na hawa wanafanya bidii kubwa kuhakikisha kuwa uongo wao unaenea kila mahali wakitumia mapokeo tu ya watangulizi wao, mazoea hayo hayaleti mabadiliko ndani yao.
  • MFANO: Bwana mmoja alikuwa akifanya usafi katika shamba lake na ndani ya shamba lake kulikuwa na chura, kobe na Kinyonga. chura alipoona kuwa mweney shamba anakaribia kuwafikia aliwahimiza rafiki zake wafanye haraka ila Kobe akajisifu kwa gamba lake akisema akinifikia nitajificha ndani. Chura akamwambia ndugu yake kinyonga, wewe huna gamba fanya haraka tutoke huku utauwawa, kinyonga akajibu akiwa katika mwendo wake wa maringo USINIHARIBIE UTARATIBU WANGU. Kila chura alipowahimiza ndiyo yalikuwa majibu yao na walipotaka kuvuka barabara chura aliona lori kubwa likija akawahimiza sana wafanye haraka ila majibu yao yalikuwa yale yale. hatimae gari liliwafikia kobe akaingia ndani ya gamba ila lilipokanyagwa lilipasuka na kinyonga nae alipokanyagwa aliharibika sana na rafiki yao Chura akiwa pembeni mwa barabara alikuwa akisikitika huku akisema laiti rafiki zangu wangenisikiliza haya yasingewatokea.
  • Wapo washarika kwa sababu ya hali za kiuwezo kiasi fulani wamejikuta wakijisahau hata wakati wa changamoto za imani hawaoni haja ya kumuomba Mungu wanaamini kuwa anawaona kama kobe.
  • Washarika wengine wamedumu katika utaratibu tu hawakubali kuona kuwa sasa ulimengu umebadilika na ibilisi anakazana kuwaangamiza, hawako tayari kuhitaji nguvu za Mungu ndani yao wanangangana na utaratibu wao.
  • Kubali leo kuacha utaratibu wako na umuombe Mungu akupe utaratibu wake.

3. UKRISTO ULIOJENGWA JUU YA NENO LA MUNGU HAUTAYUMBISHWA KAMWE

  • Mungu anauhakika na watu wake ambao neno lake limejaa ndani yao , anasema hao hawatayumbishwa na manabii wa uongo
  • Manabii wa Uongo wataendelea kudhani tu kuwa watawayumbisha ila ukweli utabaki kuwa watu waliojawa na neno la Mungu wataendelea kumwamini Mungu wa kweli

4. TUSITISHWE NA UWEPO WA MANABII WA UONGO

  • Manabii hawa wa Uongo Mungu anasema waendelee na ndoto zao na uongo wao kwani wao ni sawa na makapi, ambayo ni mepesi na yasiyo nathamani (Yer 13:24, Ayubu 21:18, Malaki 3:18) Upepo au dhoruba kali ikipita itawasambaratishia mbali.

5. NENO LA MUNGU LINA NGUVU

  • Nabii wa kweli anafananishwa na ngano safi  ambaye anasimamia neno la Mungu ambalo, kwanza linafananishwa na moto ambao hutumika kuonyesha uhalisia wa kitu (1Kor3:12-13) na kufanya utakaso (Zekaria 13:9)
  • Mtu akitaka kupata uhalisia wa kila amnachokifanya basi akipime kwa neno la Mungu
  • Mtu akihitaji utakaso wa kweli unapatikana kwa neno la Mungu tu, si kwa mafundisho ya namna fulani na miujiza fulani fulani
  • Neno la Mungu limefananishwa na nyundo iwezayo kuvunjavunja miamba ikionyesha uwezo wake wa kubadilisha mambo.

6. HITIMISHO

  • Yesu Kristo ambaye ndie Neno  ambaye katika somo la leo tumeambiwa kuwa ni moto na nyundo, anaweza kuyapima mambo yetu na pia kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha yetu, tumwalike katika maisha yetu ili tuendelee kupokea baraka zake.

AMEN.

Wednesday, 9 November 2016

KKKT: SIKU YA KUMBUKUMBU YA MATENGENEZO YA KANISA

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI
USHARIKAA WA QURUS – ENDASHANGWET

MAHUBIRI YA TAREHE 30/10/2016

SIKU YA BWANA YA KUKUMBUKA MATENGENEZO YA KANISA (Reformation)
USHUHUDA WETU

ZABURI 46, WARUMI 3:19-20, *YOHANA 3:13-17

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa wakati wote ni wakati wa matengenezo ya kanisa ili Mungu aweze kutukamilisha kwa neema yake.

UTANGULIZI
Nawasalimu wote katika jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. “Bwana Yesu asifiwe.”
Leo tunatafakari juu ya matengenezo ya Kanisa ambayo ndio ushuhuda wetu.

Ushuhuda ni maneno ya kuthibitisha na kueleza mambo yalivyokuwa au kutokea, ni uthibitisho/ushahidi.

Mungu alipoumba dunia na kuifanya kuwa kanisa lake halikuwa na haja ya matenegenezo kwa sababu aliona kila kitu ni chema (Mw 1:31) Ila baada ya anguko ndipo umuhi wa matengenezo ulipoanza kuonekana.

Ipo mifano mingi sana ya matengenezo katika Biblia ila nitataja miwili toka Agano la Kale na miwili Agano Jipya.

Matengeno ya Kanisa yalianza mara moja baada ya anguko la mwanadamu, mwanadamu alianza kuona udhaifu na Mugu akaona mtu wake anahitaji matengenezo ili aweze kuwa mwema tena ndipo Mungu aliamua kuanza matengenezo kwa kuwatengenezea Mavazi ya ngozi wanadamu wale wa kwanza kuficha udhaifu. (Mwanzo 3:21)

Tunamuona pia Yoshua alipoona kanisa la Mungu linataka kujichanganya na miungu mingine aliamua kusimama na kuonyesha msimamo kuwa Kanisa lenye michanagnyiko linahitaji kutengenezwa na liwe na msimamo mmoja ndipo aliposema mimi na nyumba yangu tutamtumikia Mungu kama ninyi mnataka kuendelea kuabudu miungu. (Yoshua 25:15)

Katika Agano Jipya kwanza tunamuona Yesu mweyewe katika somo tulilolisoma alipofika Yerusalemu na kukuta kanisa limeharibiwa na kugeuzwa kuwa soko aliamua kuleta matengenezo ya kanisa kwa kuondoa uchafu wote na wafanya biashara wote kule hekaluni. (Yn 2:13-17)

Petro nae aliamua kuyafanyia Kanisa matengenezo baada ya kuona kuwa waalimu wa uongo wameingia kanisani na kufundisha uongo ndipo aliposimama na kukemea.

Matengenezo ya Kanisa yaliendelea baadae na hata kuzaliwa kwa kanisa la Kilutheri Duniani,  sasa katika somo hili nataka ujiulize

i)                    Kwa nini wewe ni mlutheri?
ii)                  Mlutheri ni nani?

Yawezekana usiwe na majibu ya haraka ila nitakapofikia mwisho wa somo hili utapata majibu.

Kanisa letu la Kilutheri kila Jumapili ya kila mwaka mwishoni mwa mwezi wa kumi karibu na tarehe 31 huadhimisha sikukuu ya matengenezo ya kanisa yaliyofanyika tarehe 31/10/1517.
Ifikapo mwakani (2017) kanisa la kilutheri Duniani linafikisha miaka miatano(500) ya matengenezo yake, Lazima tujihoji je bado tupo kwenye msingi wa neno la Mungu au tayari tumeshatoka? Tufanye nini ili kuendeleza kazi njema ya Kuutangaza ufalme wa Mungu hapa duniani? Matengenezo haya lazima yawe ushuhuda wetu kweli katika matendo yetu na sio kinadharia tu.

USHUHUDA WETU
Kama nilivyoeleza maana ya Ushuhuda wetu mimi nina ujasiri wa kusema kuwa nimekuwa Mlutheri kwa sababu nilizaliwa katika imani hiyo nikiendelea kujiboresha kumjua Mungu zaidi.

Jina mlutheri limetokana na chimbuko toka jina la Dkt. Martin Luther, baba wa matenegenezo ya kanisa aliyekuwa na lengo la kurekebisha na kutengeneza baadhi ya mafundisho na taratibu zilizokuwa zikifanywa na kanisa la wakati ule kanisa la Kirumi(RC) ambazo zilikuwa hazijengwi kweneye msingi wa Neno la Mungu ili kurejea katika msingi wa Kibiblia.
Dkt. Martin Luther alizaliwa na kukulia nchini Ujerumani na alisoma masomo ya falsafa na sheria akiwa kijana mdogo, lakini baadae aliamua kujiunga na masomo ya Theolojia ambapo mwaka 1507 alibarikiwa kuwa padre wa katoliki na baadae alifundisha chuo cha theolojia Wittenberg. Wakati akifundisha chuoni Luher alichukizwa na mafundisho na matendo yaliyokuwa yakifanywa na Kanisa katoliki kama vile mamlaka ya papa, vyeti vya msamaha, wakristo kuzuiwa kusoma biblia nk, ndipo tar 31/10/1517 aliandika sentensi 95 kwenye mlango wa Kanisa la Wittenberg  ambazo zilizungumzia juu ya ukosefu wa elimu ya Kibiblia, matendo mabaya na kutokuwajibika miongoni mwa viongozi wa Kanisa, yeye alikuwa na lengo la kuwarejesha kwenye maandiko matakatifu.
Dr martin Luther alisimamia ukweli wa neno la Mungu katika kupambana na mafundisho potofu yaliyofanya wokovu ufikie hatua ya kununuliwa kwa hela kupitia vyeti vya msamaha pamoja na mapungufu mengine. Tunaweza kusema kuwa Luther alishuhudia ukweli wa injili kiasi cha kuwa tayari kufa kwa ajili ya ukweli pale aliposema “Hapa nasimamia ukweli wa neno la Mungu, sitabadili msimamo, nisaidie Mungu wangu”
Dkt. Martin Luther hakuwa na lengo wala nia ya kuanzisha dhehebu jipya, bali alitaka tu kusahihisha kile alichokiona kama ukiukwaji wa wazi wa mafundisho ya Biblia ila alitakiwa kukana maandishi yake ila alisema asipothibitishiwa kutoka biblia kuwa amekosea hayupo tayari kuyakanusha ndipo alipohesabiwa kuwa mzushi na kuhukumiwa Kunyongwa ila alifanikiwa kutoroka na kujificha.
Ndipo mwaka 1597 watheolojia waliokaa katika mji wa Wittenberg huko ujerumani walitafsiri jina ulutheri kumaanisha ‘Kanisa la kweli’ ambalo limejengwa kweneye msingi wa neno la Mungu ila Martin Luther alipendelea neno Kiinjili zaidi.
Mafundisho rasmi ya kilutheri ya wakati wote na mahali pote huonyesha sisi sote wenye dhambi na tunapokewa jinsi tulivyo kwa neema ya Mungu lakini hatuaswi kubaki jinsi tulivyopokelewa.(Rumi 6:1-4) na tujue kuwa ya kale yamepita tutazame mapya (1Kor 5:17) na tukazane kuzaa matunda(Mt 7:19) na huku tukiwajali wengine (Mt 25:36-46)

  • Leo hii Mlutheri anafahamika kuwa ni muumini wa dini ya Kikristo ambaye anaabudu katika Kanisa la KiinJili la Kilutheri ambalo ni ushirika wa watakatifu ambao injili inatangazwa kwa usafi na sakramenti zinatolewa kwa usahihi wake. Kama Luther alivyotafsiri maana ya Kanisa kuwa ni pale ambapo injili inahubiriwa na kupokelewa tena na saKrament ya Ubatizo na Ushirika wa Meza ya Bwana vinatolewa kwa usahihi wake.
  • Mlutheri anamwamini Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake na kubatizwa katika Utatu Mtakatifu, ambapo anasafishwa dhambi zake na kupokelewa katika kundi la waaminio na kufanyika mwana wa Mungu.
  • Mlutheri anaamini juu ya mafundisho, mafunuo, mapenzi na ahadi za Mungu kupitia maandiko matakatifu yaani Biblia, kuwa ndio msingi wa maisha yake.
  • Mlutheri anakubali na kuamini ya kuwa katekisimo ndogo ya Dkt Martin Luther, ukiri wa Nikea, Mitume, Athanasio na ungamo la Augusburg lisilobadiika ndio maelezo sahihi tena ya wazi ya neno la Mungu

KKKT imejali maisha wa kiroho ya waumini wake kwa kuzingatia Biblia na kuna vitabu vingine kama kitabu cha nyimbo TUMWABUDU MUNGU WETU pamoja na kalenda ya mwaka inayomwongoza kila mlutheri popote alipo kwa neno la Mungu kila siku asubuhi na jioni.
Nyakati hizi kumetokea mafundisho mengi sana ambayo yanawachanganya washarika wetu. Ni lazima sisi tufuate na kuenzi utaratibu wa ibada yetu ili watu waweze kutambua kuwa sisi walutheri wenye umoja na tumebobea katika mafundisho sahihi ya neno la Mungu na sakramenti zake zinatolewa kwa usafi wote
Kwa msingi wa katiba ya KKKT tunapaswa kuuenzi, kuulinda na kuimarisha umoja wetu, twapaswa sisi kushuhudia kila kona juu ya neema ya Mungu kwetu.

Waasisi wa KKKT waliweka wazi msingi wa Imani utakaofuatwa na KKKT kana ifuatavyo

KKKT lililojengwa juu ya msingi mmoja, Yesu Kristo, hukiri kwamba Neno la Mungu lililoandikwa katika Agano la Kale na Agano jipya  ndio msingi pekee wa uhakika wa Imani na maisha ya kanisa. Katika umoja wa Kanisa moja duniani, huungama ungamo la Mitume, Nikea, na la Athanasio; hukubali pia maungamo ya Kanisa la Kilutheri hasa ungamo la Augusburg lisilobadilishwa na katekisimo ndogo ya Martin Luther kuwa maelezo au mafafanuzi sahihi ya neno la Mungu. Sharika zote, na wachungaji, sinodi na dayosisi za kanisa hili zitakubali na kufuata nsingi huu wa imani.

HITIMISHO
Tunapoona habari hizi za matengenezo ya kanisa na historia nzuri za watu waliotetea imani yao hata kwa mateso yatatuhimiza sisi wa leo kuendelea kuona kuwa kanisa la Mungu linapaswa kujifunza kwa usahihi ukweli wa neno la Mungu pasipo kuyubishwa.
Tunapoona neno la Mungu linayumbishwa tusikubali hali hiyo tunapaswa kukemea kwa ukali kama alivyofanya katika hekalu ya Yerusalemu na tunapaswa kupatwa na wivu tunapoona kweli ya neno la Mungu inapindishwa.
Matengenezo ya Kanisa ni jambo endelevu ili kuendelea kupokea neema ya Mungu katika ukombozi kwenye maisha yetu.
Wapendwa washarika kwa kupitia siku hii ya matengenezo ya kanisa, tunaletewa wito wa kujenga umoja wetu katika ndoa zetu, umoja wa kifamilia, umoja wa jumuiya na sala, umoja wamitaa ya Sharika, umoja wa sharika, umoja wa jimbo, dayosisi na kanisa zima.


AMEN


Imeandaliwa na mtumwa wa Yesu Kristo Mchungaji George Mamuya


KKKT: TUDUMISHE UMOJA WA KANISA

SIKU YA BWANA YA NNE BAADA YA UTATU
 19/06/2016

WAZO: SIKU KUU YA KKKT – TUDUMISHE UMOJA WA KANISA

MASOMO” ZAB. 27:1-5, YN 17:22-23, *EFESO 4:1-4

SHABAHA: Kuwafundisha waumini jinsi umoja ulivyo na nguvu katika kufanikisha kazi ya Mungu.

UTANGULIZI: Umoja ni nguvu utengano ni dhaifu, walisema waswahili. Hata kanisa letu mwanzoni lilikuwa na makanisa saba, wakaungana chini ya mwasisis Askofu Stefano Moshi aliyewaunganisha.
Katika umoja huo kanisa liliongezeka na hatimaye mpaka sasa zipo dayosisi 24 na maeneo ya misioni 3 haya yote ni matunda ya umoja, pia ni agizo la Yesu, WOTE KUWANA UMOJA Yoh 17:21-23

Katika somo kuna mafundisho tutakayojifunza kuhusu umoja

  1. KUENENDA KATIKA WITO TULIO ITIWA
Paulo alianza kwa kuwaomba waumini waishi maisha yaliyostahili wito wao kama wafuasi wa Yesu Kristo. Anajiita mfungwa kwa sababu maisha yake yametawaliwa na Bwana.
Hata sisi ambao ni wafungwa wa Bwana maisha yetu yatawaliwe na Yesu kwani tukitawaliwa na Yesu tutashinda magumu yote kwa upendo alionao Mungu juu yetu.

  1. WAKRISTO KUISHI KAMA WATOTO WA FAMILIA MOJA YA MUNGU
Watu wa Mungu wanapaswa kushirikiana kuenenda katika wito wao walioitiwa, kuwa na maisha ya umoja na kuwa watakatifu, watu waliotofautia na watu wa dunia hii kuishi maisha safi. Hata mataifa waasiomjua Mungu wana umoja, lakini umoja unaozungumziwa hapa ni juu ya watu waliomfahamu Mungu wanapaswa kujenga umoja wao juu ya Mungu.

  1. UNYENYEKEVU NI TABIA YA MKRISTO
Yesu yeye ni mfano wa kuigwa kwani alitumika badala ya kutumikiwa. Unyenyekevu ni kinyume cha kiburi, ukiwa na kiburi unaharibu uhusiano wako na Mungu. Bali unyenyekevu ni sifa pia ni tabia impasayo mkristo. Hata sisi tunapaswa kuwa na unyenyekevu ili tuweze kutumika.

  1. UPOLE UNAJENGA UMOJA
Yesu yeye ni mpole na ni mfano wa kuigwa. Mt 11:28, katika upoole unaweza kuwasaidia watu kuishi pamoja vizuri, katika upole unaweza kujitawala kwani utakuwa umetawaliwa na Yesu na anaongoza maisha yako.

  1. KATIKA KUMTUMIKIA MUNGU UVUMILIVU UNAHITAJIKA
Mtu mvumilivu hawi rahisi kukasirika, yu tayari kuvumilia hata mabaya, yu tayari kusubiri, hafanyi haraka kutafuta haki yake. Hata sisi uvumilivu ukiwepo hata magumun yakitupata hatuko tayari kukata tama kwa ni tutavumili kwa Mungu na yeye atatupatia haki yetu.

  1. HATA KTK UDHAIFU TUNAPASWA KUCHUKULIANA KTK UPENDO
Kuchukuliana kunajenga upendo kati yetu, iwapo kuna makosa. Bila kuchukuliana hatuwezi kuonyesha upendo wa Mungu. Upendo unaunganisha waumini kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Mfano wa mwili unatajwa mwili una ushirikiano kila kiungo kikiumia mwili wote unaumia. Hivyo hata waumini pasipo ushirikiano hatutajenga mwili wa Kristo. Mwili wa kristo unajengwa katika umoja.

HITIMISHO

Kwa umoja kanisa la mwanzo liliendelea na kukua sana, hata sisi ambao tumeitwa na Mungu tutumie vema  wito wetu tulioitiwa kwa kfanya kazi ya Kristo katika kumtumikia Mungu tujivike moyo wa unyenyekevu, upole, uvumilivu, kuchukuliana, na mambo yanayofanana na hayo. Katika mambo hayo hakuna hukumu bali tunaweza kuurithi uzima wa milele. Na uzima wa milele unajengwa katika umoja unaoongozwa na Yesu. Wote tukishirikiana tutazamie kurudi kwa Yesu kristo na wote tutarajie uzima wa milele. (watumi 5:2) AMEN.


KKKT: NEEMA YA MUNGU IOKOAYO

KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI, JIMBO LA KARATU, USHARIKA WA QURUS

MAHUBIRI YA TAREHE 12/06/2016

SIKU YA BWANA YA 3 BAADA YA UTATU. RANGI YA MADHABAHU KIJANI

MADA: NEEMA YA MUNGU IOKOAYO

MASOMO: ZAB 56:1-13, TITO 3:4-8, *LUKA 8:26-39

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa ili kupata ahadi za Mungu tunapaswa kumtegemea Mungu.

“Kwa kuwa mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea” (Lk 19:10)

UTANGULIZI: Leo ikiwa ni siku ya tatu baada ya utatu tunaangalia mada izungumzayo juu ya Neema ya Mungu ambayo inatuwezesha sisi kuupata wokovu.
ü      Neema maana yake ni mafanikio aliyonayo mtu kutokana na majaaliwa ya mwenyezi Mungu au kwa juhudi zake mwenyewe.
ü      Hivyo:- tunaweza kusema kuwa leo tunazungumzia juu ya mafanikio aliyonayo mtu kutoka kwa mwenyezi Mungu ambayo yanaleta wokovu katika maisha ya mtu.
ü      Katika kutafakari Neema hii ya Mungu iletayo wokovu tumepewa kisa kutoka katika biblia Luka 8:26 – 39. Kisa hiki ambacho kimeelezwa hapa pia kimeelezwa katika kitabu cha mathayo 8:28-34 na kitabu cha Marko 5:1-20 ikizungumza habari ya mtu aliyepagawa na pepo wachafu ambao wamejitambulisha kwa jina la Legion maana yake ni jeshi kubwa la warumi lenye nguvu lililokwa na idadi ya wanajeshi 6000.
Katika kisa hiki unajifunza mambo yafuatayo:-

  1. SHETANI NI MHARIBIFU
Mtu huyu ambaye amepagawa nna pepo tunaambiwa kuwa alikuwa Uchi, aliishi makaburini, na alikuwa akijikatakata na mawe (Marko 5:3) Shetani anapoingia kwetu hahurumii hata miilil yetu atatutaabisha na kuwa wahitaji wakati wote.

  1. ULINZI WA KIBINADAMU HAUJITOSHELEZI
Mtu huyu alifungwa kwa pingu na hata kwa minyororo ila aliikata yote na wanadamu wakakata tama nay eye na kumuacha alivyo. Unaweza kutegemea wanadamu wanaweza kukusaidia ila ni kwa kitambo kidogo na utabaki katika shida yako.

  1. BINADAMU WENGI WANAANGALIA KITU KULIKO UTU
Tunaelezwa kuwa baada ya mtu huyu kuponywa watu wa mji ule walimfukuza Yesu kwa sababu walipiga hesabu ya hasara ya nguruwe 2000  waliofia majini waliona mwenzao amepata hasara kubwa sasa hawakujua nani angefuata wakaogopa sana wakaamua kumwambia aondoke kwao.

  1. MUNGU ANAJISHUGHULISHA NA MAHITAJI YETU
Yesu alivyoona kuwa mtu huyu yupo uchi, anaishi makaburini mbali na watu na alikuwa akijikata mwili kwa mawe alijua kuwa anahitaji msaada hivyo aliona nguruwe hawana umuhimu kama mtu wake akayaelekeza mapepo kwa nguruwe na kumponya yule kijana. Mapepo yalikwepa kwenda kuzimu yakidani kuwa yakiingia kwa nguruwe yatakuwa salama ila baada ya kuingia nguruwe walikufa wote na mapepo bado yakaenda kuzimu.

  1. UKIMKUBALI MUNGU UTAKUWA SALAMA
Baada ya mtu huyu kuponywa alitulia chini ya miguu ya Mungu akiwa amevaa nguo na akiwa na akili yake timamu. Amani ya kweli inapatikana kwa kumkubali Yesu


  1. MEMA ANAYOKUTENDEA MUNGU ANATAKA UMTUMIKIE
Mtu aliyeponywa alitaka kandamana na Yesu ila yesu alimwambia aende kuelezea habari njema za Yesu kwa watu wa nyumbani kwake kwa kuwa eneo lile liikuwa ni eneoo la wapagani nao waone wema wake. Baraka tunazopata tunatumwa tukahubiri.

HITIMISHO
Bora kuwa mlinzi wa getini kwa Mungu kuliko kuwa mfalme au malkia nje ya Mungu sababu huko hakuna mafanikio ya kweli, mafanikio ya kweli yaletayo wokovu yanapatikana kwa Mungu tu.


AMEN


KKKT: KUNGOJEA AHADI YA ROHO MTAKATIFU

SIKU YA BWANA KABLA YA PENTEKOSTE IITWAYO EXAUDI MAANA YAKE USIKIE KUOMBA KWETU

KICHWA: KUNGOJEA AHADI YA ROHO MTAKATIFU

MASOMO: ZAB 42:1-5, MDO 1:1-8 *YOHANA 7:37- 39

TAREHE 08/05/2016      

MAHALI: QURUS PARISH

SHABAHA: Wasikilizaji wapate kuelewa kuwa Mungu anahitaji maombi yetu apate kutusaidia.
“Bwana yu karibu na wote wamwitao, wote wamwitao kwa uaminifu.” (Zab 145:18)

UTANGULIZI: Jumapili ya leo ni jumapili inayoitwa Exaudi maana yake usikie kuomba kwetu. Siku hii inayoitwa Exaudi tumepewa kutafakari juu ya kungojea ahadi ya Roho mtakatifu. Ahadi hii iliwekwa na nani? Jibu ni Yesu Kristo mwenyewe ( Yn 16:7, Lk 24:44, Mdo 1:4, Yn 15:26). Swali kubwa kwa nini kungojea ahadi hii?
i)                    Kwa sababu Roho mtakatifu anatufungua macho ili tuweze kuelewa maana ya kifo cha Yesu msalabani, kufufuka na kupaa kwake ktk utukufu na siku ya pentekoste (Yn 16:14)
ii)                  Roho mtakatifu huja ndani yetu na kutu zaa mara ya pili ili kupata msamaha wa dhambi, wokovu ns uhuru (Yn 3:3-7)
iii)                Roho mtakatifu anabadili maisha yetu na kuleta utakaso kila siku (2kor 3:18, 1Thes 4:10)

  • Katika kungojea ahadi hii nzuri katika maisha yetu leo tumepewa kutafakari (Yn 7:37-39)
  • Wayahudi walikuwa na sikukuu tofauti tofauti za kiimani, mojawapo ya sikukuu hizo ilikuwa sikukuu ya vibanda, sikukuu hii ilikuwa inadumu kwa siku saba na walikuwa wanakaa katika nyumba za nyasi za muda waliojitengenezea, sikukuu ilikuwa ni siku ya kukumbuka maisha yao ya jangwani na pia ilikuwa ni sikukuu ya mavuno kumshukuru Mungu(Law 23:33,Kumb 16:13-15) na zilitolewa sadaka mbalimbali (Hes 29:12-18)
  • Kipindi cha Yesu nae alihudhuria sherehe hizi na siku ile ya mwisho alipata nafasi ya kusema maneno tuliyosoma (Yn 7:37-39)
  • Katika maneno haya aliyoyasema Yesu alipenda tujifunze au tufahamu kuwa:-


  1. KILA MHITAJI AMUENDEE YEYE ATAPOHEA HITAJI LAKE.
  • Yesu alitumia mfano wa maji ili wayahudi waweze kuelewa vizuri walipokumbuka maji yaliyotoka kwenye mwamba wakiwa jangwani wazee wao walipokuwa na kiu (Kut 17:1-7)
  • Kiu ni hali ya uhitaji au shauku ya kupata jambo Fulani
  • Yesu anatoa mwaliko hu, Jew ewe una kiu ya aina gain? (uhitaji wa aina ipi?)
  • Lile ambalo linatesa maisha yako na unahitaji msaada Yesu anasema lilete kwangu atakupa ufumbuzi. Ni tatizo la ndoa, magonjwa, dhiki mbalimbali, dhuluma,dhambi imekulemea nk yote uyalete kwake yatakuwa yamepata ufumbuzi. Wewe endelea kumuamini tu.


  1. IMANI YETU YAPELEKEA SISI KUJAZWA ROHO MTAKATIFU
Yesu altumia mfano wa maji yakitiririka akionyesha wazi kuwa wote watakaomwamini watajazwa nguvu za Roho mtakatifu na wataweza kufanya mambo makubwa ya ufalme wa Mungu hapa duniani na kuweza kumshinda shetani na ufalme wake wote, pengine alikumbuka neno toka Yoel 2:28 – 29 ambalo limejirudia Mdo 2:16-21

  1. HITIMISHO
Sote tunapaswa kutamani kuona mapenzi ya Mungu ndani yetu na ndani ya ulimwengu huu kwa ujumla na kumuamini yeye kuwa ndie muweza wa mambo yote ili tujazwe nguvu za Roho mtakatifu aliyemsaidizi wetu ili tuweze kutembea vyema kwenye ulimwengu huu na hatimaye tuurithi uzima wa milele. 

AMEN

Yameandaliwa na Mch. George Mamuya


KKKT: AMEPAA KATIKA UTUKUFU WAKE

SIKU YA KUKUMBUKA KUPAA KWAKE YESU KRISTO
MADA: AMEPAA KATIKA UTUKUFU WAKE
MASOMO: ZABURI 110, YOHANA 16:28 -33, *WAKOLOSAI 3:1 – 4
TAREHE 05/05/2016     MAHALI: QURUS PARISH

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa wanapaswa kumtegemea Mungu.

UTANGULIZI: Siku ya leo alhamisi tunakumbuka siku ya kupaa kwake yesu Kristo kwenda mbinguni. Tunapokumbuka siku hii tunakumbuka alitoa ahadi kuwa anakwenda kutuandalia makao, atatuletea Roho mtakatifu na alitupa maagizo ya kwenda kuwafanya watu wote wa ullimwengu kuwa wanafunzi wake kwa kuwabatiza katika Utatu wa Mungu.
Mada kubwa ikisema kuwa alipaa katika utukufu wake. Neno Utukufu lina maana ya heshima sana, Heshima hii inapatikana baada ya kazi nzito ya kuukomboa ulimwengu, heshima haiji kirahisi lazima mtu kutokwa jasho ili kuipata heshima hiyo.
Siku hii tumepewa kuangalia mistari mine toka kitabu cha wakolosai 3:1-4 ambapo tunajifunza mambo yafuatayo

  1. UBATIZO NI MUHIMU SANA KWA MAISHA YA MKRISTO
  •  Kitendo cha ubatizo ni kitendo cha nje tu kinachoonyesha kuwa huyo aliyebatizwa amekufa pamoja na Kristo kwa maisha ya nyuma(dhambi) nay a kuwa amefufuliwa na kristo kwa maisha mapya.
  • Umuhimu wa ubatizo kwetu ni kuwa huutoa msamaha wa dhambi ( mdo 2:28, 22:16b), huokoa kutoka mautini na kutupatia uzima wa milele na kutuokoa toka kwa ibilisi (Rum 6:3,5, Gal 3:27, Kol 1:13-14, mk 16:16a, 1Pet 3:21, Tit 3:5b)
  • Hivyo tunapaswa zaidi kuviangalia vile vya juu aliko Yesu Kristo vile amabavyo havionekani sio vile vinavyoonekana kwa sababu hata kama miili yetu ikichakaa lakini roho zetu zinaendelea kufanywa mpya kila siku (2Kor4:16-18)


  1. UKRISTO NI MAISHA YA KIELELEZO
  • Tunapaswa kutumia maisha yetu kutafuta yale yanayompendeza Mungu.
  • KUTAFUTA ni kupekuwa huku na kule ili kuona kitu unachokitaka au kilichopotea
  • Hivyo tunapaswa wakati wote kupekua kila mahali kutafuta mapenzi ya Mungu na kuokoa kile ambacho kimepotea
  • Na sio kutafuta tu bali pia tunapaswa kufikiri
  • KUFIKIRI ni kuwaza kwa kutumia akili ili kuelewa jambo au kitu kabla ya kufanya maamuzi
  • Ukristo wetu sio wa kukurupuka tunapaswa kutumia akili na kufikiria sana jinsi tunavyoenenda je ni kweli tunampendeza Mungu? Tunafanya mapenzi yake? Tunakuwa kielelezo kwa watu wengine? Kama sivyo tujitahidi kutenda hayo tukiomba uongozi wa Roho Mtakatifu.


  1. TAFUTA ZAIDI KUFANYA MAPENZI YA MUNGU, WATU WATAELEWA TU HATA KAMA SIO SASA
Wakati mwingine tunapofanya mambo ya rohoni watu wengine wanaweza wasielewe na hata kukuona mtu wa ajabu ila usihofu kwa sababu wakati wa kufunuliwa utakapofika watakuelewa tu tena utafunuliwa kwa heshima kuu, wewe endelea tu kupalilia heshima yako kwani kumtegemea mwanadamu huleta mtego (Mithali 29:25)

  1. HITIISHO
Maisha yetu yanapata thamani pale tunaposhikana na Yesu Kristo, kwani yeye tulikufa nae ktk dhambi zetu, tukafufuka nae katika upya wa maisha yetu na tutafunuliwa pamoja nae sisi tuendelee tu kumwamini na kumtegemea yeye.
AMEN


Yameandaliwa na Mch. George Mamuya

Mzee Emanuel akishiriki sakramenti ya meza ya Bwana.