SIKU YA BWANA YA SABA KABLA YA PASAKA
ZABURI 123:1 - 4, 2KORINTHO 11: 23 - 30, *LUKA 18: 31 - 34
TAREHE 26/02/2017
"Nanyi mnafahamu kwamba, Mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au kwa dhahabu, mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu, bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana - kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo" (1Petro 1:18 - 19)
UTANGULIZI
- Mungu aliye mwema sana kwetu kwa neema yake leo ametupa kibalil cha kulitafakari neno lake toka Luka 18: 31 - 34 linalozungumzia safari yake ya kwenda Yerusalemu
- Safari ya Yerusalemu ni muhimu sana kwetu na kwa Yesu Kristo. Kwa Yesu kwa sababu anakamilisha lengo lake la kimkomboa mwanadamu. Na Kwetu sisi wanadamu ni muhimu sana sababu kwa kukamilika kwa lengo la Yesu sisi tunakombolewa toka katika mikono ya shetani.
- katika safari hii ya kwenda Yerusalemu ndipo Yesu anatabiri kwa mara ya tatu juu ya mateso yake na kifo chake na ufufuko wake.
- Habari hii pia inapatikana katika injili nyingine (Mathayo 20;17 - 19, Marko 10:32 - 34) ambapo katika habari hii tunajifunza mambo yafuatayo
1. UHUSIANO MZURI NA MUNGU UNATUFUNULIA MAMBO YATAKAYOTOKEA.
- Yesu alipokuwa akiwahudumia na kuwafundisha watu wengi ulipofika wakati wa kutaka kusema yatakayotokea baadae aliwatenga faraghani wanafunzi wake na kuwaeleza habari za yeye kwenda Yerusalemu na kuteswa, kuuwawa na kufufuka.
- Tunapaswa sisi wote tuliochaguliwa na Yesu kwa neema yake tutafute ukaribu na uhusiano mzuri naye kwa nia ya toba kama alivyosema katika mathayo 4:17 "Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri akisema, tubuni kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia" ili tuweze kupatiwa siri za kimbingu tuweze kumshinda shetani na kuurithi uzima wa milele.
2. NGUVU NA UMAARUFU WETU USIPOFUSHE MACHO NA MASIKIO YETU YA KIROHO
- Wanafunzi walipoelezwa habari ya Mambo yatakayotokea Yerusalemu tunaambiwa kuwa hawakuelewa maneno hayo hata kidogo.
- Walikuwa karibu na Yesu sawa, walikuwa na imani sawa, lakini hawakuelewa neno lolote
- Kwanini Hawakuelewa? Jibu lake kulingana na kifungu tulichosoma unaweza kunijibu kwa sababu yalikuwa yamefichwa kwao. Ni sawa
- Swali hili linahitaji Muda kulitafakari na kumuomba Mungu akufunulie. Yaweza kuwa Mungu alitaka yatakapotokea hayo wakumbuke na utukufu wake uwe mkuu ama sababu ya pili ianatokana na wanafunzi wake.
- Kwanza wanafunzi kwa kuona mambo yaliyokuwa yanafanywa na Yesu, nguvu alizotumia, na umaarufu walioupata kwa kipindi kile walijua wakifika Yerusalemu watakuwa watawala, ndio maana Yakobo na Yohana walimuomba Yesu wakae mkono wa kuume na mwingine mkono wa kushoto na wale wenzao walikuwa na mawazo kama hayo na waliposikia wakakasirika (Marko 10:35 - 42)
- Pili hawakuwa tayari kuamini wala kukubaliana na ukweli wa mateso yatakayotokea "Petro akamchukua akaanza kumkemea akisema, hasha, Bwana, hayatakupata"(Mt 16:22)
- Je, ni mara ngapi nguvu na umaarufu wetu umetufanya tusikubali kweli ya neno la Mungu?
- Je, ni mara ngapi mambo ya kidunia yametufanya tushindwe kuamini kweli ya neno la Mungu?
- Yawezekana kabisa kuwa Mungu anaongea nasi mara kwa mara lakini tunashindwa kumuelewa wala kumuamini kwa sababu tu ya mawazo yetu ya kibinadamu yanayofanya macho yetu ya kiroho yasione wala masikio yetu yasisikie
- Yawezekana ni nguvu zetu, umaarufu wetu, utajiri wetu, elimu yetu, cheo chetu ndivyo vinavyotufanya tusielewe kweli ya neno la Mungu.
- Vitu vyote nilivyotaja hapa ni vitu vya baraka sana kwetu na kwa kanisa kama vikitumika kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
- Nguvu uliyonayo, umaarufu ulionao, utajiri ulio nao, elimu uliyo nayo, cheo ulichonacho badala ya kujivuna navyo, umuulize Mungu anataka uvifanyie nini kwa ajili ya utukufu wake
- Vitu hivi tukivifanya si chochote mbele za Mungu na kutambua kuwa Mungu ndie asili ya kila kitu basi itakuwa rahisi kwetu kuisikia sauti ya Mungu na kuielewa.
3. MATATIZO YASIKUONDOE KWENYE LENGO
- Lengo la Yesu Kwenda Yerusalemu ilikuwa ni kuumkomboa mwanadamu, japo alitambua atafanyiwa dhihaka, atatendewa jeuri, atatemewa mate, atapigwa mijeledi, atauwawa, hayo yote hayakuweza kufanikiwa kumuondoa Yesu kwenye lengo lake la kumkomboa mwanadamu, alitambua baada ya hayo atashinda kwa kiasi kikubwa kwa kufufuka na kumpatia ukombozi mwanadamu aliyeasi na kutengwa mbali na uso wa Mungu.
- Wakristo wa leo tunayosafari ya kuuendea uzima wa milele kwa kupitia wokovu wa milele kwa kumwamini Yesu aliyetupatia ukombozi kwa njia ya msalaba "naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii" (Ebr 5:9)
- Safari hii ya kuelekea uzima wa milele inatupatia maisha ya baraka hapa duniani na baadae uzima wa milele "ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba,na ndugu waume, na ndugu wake, na mama na watoto, au mashamba, pamoja na udhia na katika ulimwengu ujao uzima wa milele"(Mk 10:30)
- Safari hii nayo ina mateso yake, Je mateso hayo yamekuondoa kwenye lengo? Mateso haya yanaweza kuwa kunyanyaswa, kuonewa, kudhalilishwa, kuchukiwa, kupigwa na hata magonjwa. haya yote yanaweza kuwepo lakini yasikuyumbishe imani yako, wewe ngangana tu kwenye lengo la kuuridhi uzima wa milele.
4.HITIMISHO
- Je, kuna kitu ambacho kimekutenga wewe mbali na uso wa Yesu na usiweze kusikia sauti yaku?
- Je, kuna hali yoyote ya kuviangalia vitu vya dunia hii vinavyoharibika na kuacha kusikia sauti ya Mungu?
- Je kuna mambo yaliyotokea ambayo yameondoa kwenye lengo lako la uzima wa milele?
Tumuombe Mungu kwa neema yake tuweze kuboresha uhusiano wetu na yeye na kuyatafuta mapenzi yake ili tuweze kusikia na kuelewa neno lake na kusimama kwenye lengo letu la kupata uzima wa milele.
AMEN.
Barikiwa sana mtumishi wa Mungu nimejifunza jambo jema Amen
ReplyDeleteBarikiwa sana Mtumishi. Nimepata cha kwenda kufundisha jumapili ijayo kwenye jumuia.
ReplyDeleteMungu akubariki sana!
TAZAMENI TUNAPANDA KWENDA YERUSALEMU.
Umeongea sahihi maana hili somo naliona gumu kweli kweli, lakini hata mimi nimepata mwanga wa kwenda kufundisha jumuiya yangu
Delete