SIKU YA BWANA YA 8 KABLA YA PASAKA
ZABURI 118: 23 - 29, MARKO 4:1- 9, *YEREMIA 23:24 - 29
TAREHE 19/02/2017
UTANGULIZI
- Ashukuriwe Mungu ambaye kwa neema yake leo ametupa kujifunza neno lake, huku tukikumbushwa kuwa "Neno la Mungu lina Nguvu"
- Neno la Mungu si jambo fulani lililoandikwa au kusemwa tu, bali ni jambo lililofanya mambo, ndani ya neno mlikuwa na nguvu ya Mungu.
- Neno la Mungu ni nafsi iliyo hai. (Yohana 1:1 - 4,14)
- Neno la Mungu lililosemwa liliandikwa na neno ni nafsi ya Yesu na ni hai nalo linafanya kazi (Ebr 4:12)
- Na leo tunaangalia neno kutoka Yeremia 23:24 - 29, ambayo ni sehemu ya nne katika mfululizo wa mafundisho juu ya nabii wa uongo katika kitabu hiki cha Yeremia mlango wa 23, ambapo sehemu hizo ni
- Sehemu ya kwanza 23:9 - 12
- Sehemu ya pili 23:13 - 15
- Sehemu ya tatu 23:16 - 22
- Sehemu ya nne 23:23 - 32
- Sehemu ya tano 23:33 - 40
- Katika sehemu hii ya nne mwandishi anatuonyesha juu ya uwepo wa manabii wa uongo ns msnsbii wa ukweli
- Manabii wa uongo wanaongozwa na ndoto na akili zao wakizingatia mazoea na miujiza
- Manabii wa ukweli wanaongozwa kwa neno la Mungu
- Katika soo hili tunaona mambo haya muhimu
1. MUNGU YUPO KILA MAHALI
- Hakuna mwanadamu anayeweza kujificha Mungu asimuone awe ni mtu mwema au asie mwema, wote anawaona.
- Anayetenda mabaya au mema ajue kuwa Mungu anamuona na atalipwa kulingana na matendo yake hivyo mtu asijifariji katika kutenda mabaya kisa tu hajaona Mungu anamuadhibu waziwazi. jua unaonekana na utalipwa kulingana na mwenendo wako
2. SI KILA ANAYETAJA JINA LA MUNGU ANAFANYA MAPENZI YA MUNGU
- Mungu anasema manabii wa uongo wanatumia jina lake kuendeleza uongo wao ili waweze kukubalika mbele za watu, wanayasema maneno ya Mungu huku wakijidanganya wenyewe na kuwadanya wengine wafanane nao
- Na hawa wanafanya bidii kubwa kuhakikisha kuwa uongo wao unaenea kila mahali wakitumia mapokeo tu ya watangulizi wao, mazoea hayo hayaleti mabadiliko ndani yao.
- MFANO: Bwana mmoja alikuwa akifanya usafi katika shamba lake na ndani ya shamba lake kulikuwa na chura, kobe na Kinyonga. chura alipoona kuwa mweney shamba anakaribia kuwafikia aliwahimiza rafiki zake wafanye haraka ila Kobe akajisifu kwa gamba lake akisema akinifikia nitajificha ndani. Chura akamwambia ndugu yake kinyonga, wewe huna gamba fanya haraka tutoke huku utauwawa, kinyonga akajibu akiwa katika mwendo wake wa maringo USINIHARIBIE UTARATIBU WANGU. Kila chura alipowahimiza ndiyo yalikuwa majibu yao na walipotaka kuvuka barabara chura aliona lori kubwa likija akawahimiza sana wafanye haraka ila majibu yao yalikuwa yale yale. hatimae gari liliwafikia kobe akaingia ndani ya gamba ila lilipokanyagwa lilipasuka na kinyonga nae alipokanyagwa aliharibika sana na rafiki yao Chura akiwa pembeni mwa barabara alikuwa akisikitika huku akisema laiti rafiki zangu wangenisikiliza haya yasingewatokea.
- Wapo washarika kwa sababu ya hali za kiuwezo kiasi fulani wamejikuta wakijisahau hata wakati wa changamoto za imani hawaoni haja ya kumuomba Mungu wanaamini kuwa anawaona kama kobe.
- Washarika wengine wamedumu katika utaratibu tu hawakubali kuona kuwa sasa ulimengu umebadilika na ibilisi anakazana kuwaangamiza, hawako tayari kuhitaji nguvu za Mungu ndani yao wanangangana na utaratibu wao.
- Kubali leo kuacha utaratibu wako na umuombe Mungu akupe utaratibu wake.
3. UKRISTO ULIOJENGWA JUU YA NENO LA MUNGU HAUTAYUMBISHWA KAMWE
- Mungu anauhakika na watu wake ambao neno lake limejaa ndani yao , anasema hao hawatayumbishwa na manabii wa uongo
- Manabii wa Uongo wataendelea kudhani tu kuwa watawayumbisha ila ukweli utabaki kuwa watu waliojawa na neno la Mungu wataendelea kumwamini Mungu wa kweli
4. TUSITISHWE NA UWEPO WA MANABII WA UONGO
- Manabii hawa wa Uongo Mungu anasema waendelee na ndoto zao na uongo wao kwani wao ni sawa na makapi, ambayo ni mepesi na yasiyo nathamani (Yer 13:24, Ayubu 21:18, Malaki 3:18) Upepo au dhoruba kali ikipita itawasambaratishia mbali.
5. NENO LA MUNGU LINA NGUVU
- Nabii wa kweli anafananishwa na ngano safi ambaye anasimamia neno la Mungu ambalo, kwanza linafananishwa na moto ambao hutumika kuonyesha uhalisia wa kitu (1Kor3:12-13) na kufanya utakaso (Zekaria 13:9)
- Mtu akitaka kupata uhalisia wa kila amnachokifanya basi akipime kwa neno la Mungu
- Mtu akihitaji utakaso wa kweli unapatikana kwa neno la Mungu tu, si kwa mafundisho ya namna fulani na miujiza fulani fulani
- Neno la Mungu limefananishwa na nyundo iwezayo kuvunjavunja miamba ikionyesha uwezo wake wa kubadilisha mambo.
6. HITIMISHO
- Yesu Kristo ambaye ndie Neno ambaye katika somo la leo tumeambiwa kuwa ni moto na nyundo, anaweza kuyapima mambo yetu na pia kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha yetu, tumwalike katika maisha yetu ili tuendelee kupokea baraka zake.
AMEN.
0 comments:
Post a Comment