Monday, 3 October 2016

ELEKEZA HOFU YAKO SEHEMU SAHIHI.

ELEKEZA HOFU YAKO SEHEMU SAHIHI (MITHALI 29:25)
"Kuwaogopa wanadamu huleta mtego; Bali amtumainie BWANA atakuwa salama."
"Maisha ya mwanadamu wakati mwingi yametawaliwa na hofu, ama kwa wanadamu wenzake, shetani au kwa Mungu. Leo nataka kuonyesha wazi kuwa mwanadamu kuwa na hofu ni kitu cha kawaida ila kuna sehemu ambayo ukielekeza hofu yako kweli utakuwa umeielekeza sehemu sahihi na maisha yako yatakuwa salama.


  • Neno hili nililolichagua kutoka biblia linatuambia hofu juu ya mwanadamu huleta mtego ambao una uangamivu kwa maisha yako.
  • na kwa upande wa pili neno hili linatueleza kuwa tukielekeza hofu yetu kwa Mungu basi Mungu anatuhakikishia usalama na kutuimarisha wakati wote kwa kutuambia USIOGOPE kwa sababu kwake utakuwa salama wakati wote (Mithali 18:10) "Jina la BWANA ni ngome imara; mwenye haki hukimbilia, akawa salama." 
  • Hofu juu ya mwanadamu hutuondolea ukaribu wetu na Mungu na hata kusababisha laana kwetu. ( Rumi 12:1-2)
  • Harunu aliwaogopa wanadamu akatengeneza sanamu matokeo yake akawatenga watu na upendo wa Mungu (Kutoka 32:22-24)
  • Mfalme Sauli alipoteza Ufalme wake kwa kuwaogopa wanadamu na kumuacha mfalme Hagai akiwa hai (1 Samweli 15:24)
  • Herode aliwaogopa watu akamuua Yohana Mbatizaji japo hakutaka (Matayo 6:6-11)
  • Pilato naye alihofia kuharibika kwa uhusiano wake na watu aliowaongoza akamtoa Yesu (Yohana 19:11-16)
  • Petro naye alimkana Yesu kwa kuwaogopa watu ( Mt 26:60-75)
  • Petro kwa kuwaogopa watu alipunguza uwezo wake wa kuhubiri asije akawakwaza (Wagalatia 2:11-13)
Tumeona sehemu tu ya watu ambao waliweka hofu kwa wanadamu na kujikuta wanaendelea kuwa mbali na Mungu.

Wote ambao wameweka hofu yao juu ya Mungu wamejikuta wakati wote wakiwa salama


  • Daudi hakuogopa ndugu zake walipomtishia na kumwambia kuwa hataweza kupambana na Goliati ila yeye alipuuza maonyo hyo na kuweka tumaini lake kwa Mungu akaweza kumshinda Goliati (1 Samweli 17:28)
  • Daudi hakumuogopa Mfalme Dario wala tundu la Simba na Mungu aliweza kumlinda akawa salama (Daniel 6:10)
  • Kijana Shedrack na wenzake hawakumuogopa mfalme Nebkadreza na watu wake Mungu akwaokoa (Daniel 3:16-18)
  • Siku ya Pentekoste mitume wa Yesu waliweka wazi kuwa wanapaswa kumuogopa Mungu peke yake (Mdo 5:29)
  • Yusufu aliomba mwili wa Yesu kwenda kuuzika bila hofu kwa wanadamu na akafanikiwa (Marko 15:43)
Maelezo haya yanakuonyesha wazi kuwa hofu uliyonayo wewe unapaswa kuielekeza wapi, Jibu nadhani utasema ni pale ambapo ukiielekeza mwisho wake unakuwa salama.

Ili kuielekeza hofu yetu mahali salama sisi kama wakristo tunapaswa kufanya nini?
  1. Kuliamini neno la Mungu (Ayubu 32:6-14, Zaburi 119:100, Isaya 8:20)
  2. Jiepushe na Marafiki waovu (Mithali 9:6; 22:24 - 25, Zaburi 101:3, 1Korintho 15:33)
  3. Amini kuwa Mungu anakulinda ( Daniel 3:16-18, waebrania 13:6)
  4. Tambua kuwa wanadamu ni dhaifu na wanahitaji msaada toka kwa Mungu umtegemee (Zaburi 39:5; 62:9, 1Timotheo 6:20)
  5. Kutafuta umaarufu, kukubalika, kusaka upendeleo kwa wanadamu ili kukwepa kutengwa na kukataliwa hilo ni chukizo mbele za Mungu. Tafuta tu yote kwa Mungu na yeye atayadhihirisha katika ulimwengu wa mwili.
HITIMISHO
Fahamu wazi kuwa unapofanya mapenzi  ya Mungu na kupenda ukweli kuna vipindi utatengwa na hata kukataliwa ila kumbuka kama waliweza kumchukia, kumtenga, kumkataa na hata kumuua Yesu sembuse wewe?(Yohana 15:18-25) ila usisahau kuwa neno la Mungu linatuhakikishia kuwa tukimtumaini Mungu atatupigania na wala hakuna silaha itakayoinuka juu yetu na kutudhuru. "Kila silaha itakayoinuka juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA." (Isaya 54:17)

Mchungaji George Mamuya

AMEN.

0 comments:

Post a Comment